MAHUBIRI YA SHEREHE YA PENTEKOSTE MWAKA A WAKANISA: ROHO MTAKATIFU HULITAKATIFUZA KANISA




MAHUBIRI YA SHEREHE YA PENTEKOSTE MWAKA A WAKANISA: ROHO MTAKATIFU HULITAKATIFUZA KANISA
MASOMO
Somo I: Acts 2:1-11
Somo II: 1Cor 12:3b-7, 12-13
Injili: John/Jean 20:19-23
SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, kwa ushirika wa Yesu Mkombozi wetu na kwa uwepo na nguvu ya Roho Mtakatifu, Kanisa lako lilitakatifuzwa, basi ee Baba tunakuomba, utusaidie sisi viungo vya Kanisa lako kusudi tubaki waaminifu kwa kulishika Neno na Amri yako. Uwatakase na kuwalinda Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amen. 
UTANGULIZI
Taifa la Mungu, SHALOOM: wapendwa leo tunao furaha ya kuhitimisha mahadhisho ya sherehe ya Pasaka ambalo kiliturgia leo tunahesabu siku 50 tangu tulipoanza kusherekea mafumbo ya wokovu wetu yaani: Kuteswa, Kufa, Kufufuka na Kupaa Mbinguni Bwana wetu Yesu: Ndio sababu leo ni Sherehe ya Pentekoste maana yake ni “siku ya hamsini”.(50th) Ni siku ya hamsini tangu tulipo sherehekea Jumapili ya Pasaka yaani Jumapili ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo: Basi kwa namna ya pekee Katika Sherehe tunakumbuka kwanza ujio wa Roho Mtakatifu kwa Mitume, tunakumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa utume wa Kanisa. Na pili, Mama Kanisa uweka Sherehe hii kuwa Sherehe ya waamini walei wote.(feast of lay people or la fête des laics) Kwa hiyo, tukiwa na dhamira hiyo tutafakari kuusu Roho Mtakatifu Katika Maisha yetu na Katika Kanisa letu.
UFAFANUZI
Wapendwa katika Kristo, wengi kati yetu uwa najiuliza kila mwaka kwa nini sherehe ya Pentecoste? neno Pentecoste limetoka wapi na asili yake ni nini ? na ni kwa sababu gani Kanisa letu usherekeya siku hiyo kama Mwanzo wa Kanisa na ujio wa Roho Mtakatifu? Bila shaka tunasehemu mbili ambao inatupa ufafanuzi wa matukio kama haya katika safari ya imani na wokovu wetu : Sehemu ya kwanza bila shaka ni Biblia Takatifu na sehemu ya pili ni historia ambao ufasiria vizuri maisha fulani ya watu fulani, na kwa namna ya pekee kuusu swali letu ni historia ya wana teule wa Mungu yaani wa Israeli. Wapendwa katika Kristo, basi mimi leo napenda kuchukua sehemu ya kwanza ambao ni Biblia kusudi niwaelekeze kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu limbuko, asili ya sherehe hii ya Pentecoste.
Kwanza nivizuri kutambuwa kwamba sherehe ya Pentecoste inatoka kwa Mungu wetu Mwenyewe wala sio kwa maneno ya wanadamu. Tukisoma kitabu cha MAMBO YA WALAWI(Leviticus au Levitique) sura ya 23 tutaona wazi namna gani Mungu kupitia Musa, anawapa wana wa Israeli sikukuu za israeli ambalo ni sikukuu zake Mwenyewe : Tusome Walawi sura 23 :1-2 : Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, sikukuu za Bwana, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu, hizi ni sikukuu zangu. Kwa hiyo ukiendelea kusoma mustari ama verset ile ya 3 hadi ile ya 44 utakuta sikukuu mbali mbali za Mungu ambalo huwapa wana wa Israeli kuwa sikukuu muhimu kabisa katika maisha yoa : ni kama vile sabato(Walawi 23,3-4), Pasaka ya Mkate usiotiwa chachu (Walawi 23,5-8), Mganda wa Malimbuko(Walawi 23,9-14), siku ya kwanza kisha mwezi wa saba(Walawi 23,23-25), siku ya Upatanisho(Walawi 23,26-32), sikukuu ya vibanda(Walawi 23,33-44) na sikukuu ya majuma ambao ni sikukuu ya Pentecoste ya wayahudi.(Walawi 23,15-22)
Maana yake, sikukuu ya Petencoste kwanza asili yake nikutoka kwa wayahudi ambao waliomriwa kuhadhimisha sikukuu hiyi(soma Waliwa 23, 15-22) siku 50 baada ya pasaka ya Kiyahudi ambamo kwa wayahudi Pentecoste ao sikukuu ya majuma ao ya Mavuno : ni siku ya Kumshukuru Mungu kwa kutoa sadaka ya mavuno yao, vifugo vyao na vitu vingine kwa ukumbusho wa ukombozi wao ambao ufamika kama pasaka ya kwanza yaani pasaka ya  Kiyahudi. Katika sherehe hiyo wayahudi uwa natoka sehemu ao nchi tafouti (wakiongea lugha mbali mbali ambao walijiufunza huko waliko toka) na kuelekea Hekaluni Yerusalemu kusudi kumpa Mungu shukrani…
Basi kwa kifupi : Pentecoste (ilikuwa) ni sikukuu ya wakulima ambao baada ya kuvuna mazao yao ya kwanza, walimshukuru Mungu kwa yale waliyojaliwa na papo hapo kumwomba awajalie tena mavuno mema msimu ufuatao. Ndiyo maana iliitwa sikukuu ya mavuno. Iliitwa pia sikukuu ya majuma kwa vile ilisherehekewa majuma machache tu baada ya pasaka ya Wayahudi. Hivyo ina maana kwamba Sherehe hii ilianza baada ya kuwekwa rasmi tarehe maalumu ya Pasaka ya Wayahudi, kwani wahusika wa Sherehe hii walikuwa ni Wayahudi au Waisraeli. Kadiri ya muda ulivyoendelea, polepole sherehe ya Pentekoste ilipata maana mpya ambayo ni ya kidini. Waisraeli walianza kuadhimisha sherehe ya Pentekoste kama ukumbusho wa siku Musa alipopewa amri kumi za Mungu mlimani Sinai. Ni siku hiyo ambapo Taifa la Israeli lilizaliwa kwa kupewa kanuni rasmi za kuwaongoza, yaani Amri za Mungu. Sherehe hiyo sasa ilichukua sura mpya ikiwakumbusha tukio kubwa na la maana sana kwao yaani kuzaliwa kwa Taifa lao la Israeli. (tusome Kutoka 19)
Sasa tukiwa na picha ya sherehi ya kiyahudi na baada ya kuelewa maana halisi ya sikukuu ya Pentecoste ya wayahudi basi tutaelewa pia mahadhimisho ya sikukuu hii ya leo kwetu sisi wakristu. Kwa hiyo mama Kanisa kupitia mafundisho ya mtaguso wake wa Pili ama council Vatican II utufundisha kwamba: Kila wakati na katika kila taifa mtu amchaye Mungu na kutenda haki hukubaliwa na yeye (tusome Acts10, 35). Lakini ilimpendeza Mungu kuwatakatifuza na kuwaokoa watu, siyo mmoja mmoja na pasipo muunguno kati yao, bali kwa kuwaunda kama taifa moja, lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia kitakatifu. Kwa hiyo alijichagulia watu wa Israeli kuwa taifa lake, akafunga agano na taifa hilo, akalifundisha polepole kwa kujidhihirisha katika historia yake yeye mwenyewe na kufunulia  kusudio la mapenzi yakke, naye akaliweka wakfu(consacré au consecrated) kwa ajili yake. Lakini hayo yote yalitokea kama matayarisho na mfano wa lile agano lililo jipya na kamilifu ambalo lilitakiwa kufungwa katika Kristo, na wa ule ufunuo mtimilifu wa kuletwa na Neno wa Mungu mwenyewe aliyejifanya mwili(haya mafundisho tunayapata katika Konstitusio ya Kidogma juu ya Fumbo la Kanisa ukurasa wa 9)

Kumbe sasa sherehe ya Pentecoste ya wakristu ni bila shaka ukumbusho wa siku 50 baada ya kukombelewa na Yesu kutoka utumwa wa dhambi a mauti na pia kukusanya naye kwa upewa wa nguvu ya Roho Mtakatifu kuwa Taifa mpya yaani Kanisa ambao Kristo Mwenyewe ni Kichwa cha Kanisa hilo mpya. Ndio sababu mafundisho ya Kanisa hutuimiza ya kuwa: Pale ilipotimilika kazi Baba aliyomkabidhi Mwana afanye duniani (tusome Yohane 17,4), basi Roho Mtakatifu akatumwa siku ya Pentecoste ili kulitakatifuza Kanisa siku hadi siku, na waamini wapate njia ya kumkaribia Baba kwa Kristo katika Roho mmoja( somo Eph au Waefeso 2,18). Huyu ndiye Roho wa uzima au chemchemi ya maji yabubujikiayo uzima wa milele.(tusome Yohane 4,14 pia 7, 38-39). (haya mafundisho tunayapata katika Konstitusio ya Kidogma juu ya Fumbo la Kanisa ukurasa wa 4)
Ndio maana wapendwa, masomo yetu yote 3 ya leo utuonesha wazi Mwanzo wa Kanisa na Kazi ya Roho Mtakatifu kaitka kulitakatifuza Kanisa hilo na waamini wake wote siku hadi siku. Wengi wanaweza sasa kujiuliza: Kanisa lilianza siku gani au lini? Rasmi, tunaweza kusema kwamba Siku ya Pentecoste ni siku ya kuzaliwa kwa Kanisa yaani Taifa mpya ya Mungu: lakini nivizuri kufahamu kwamba Bwana Yesu alianzisha Kanisa lake kwa kuihubiri habari njema, yaani ujio wa ufalme wa Mungu, ulioahidiwa tangu karne nyingi katika maandiko: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili” ( tusome Marc 1,15 na Mathew 4,17). Basi ufalme huo unang’aa wazi mbele ya watu katika Neno la Kristo, katika matendo yake na uwepo wake.
Kwa hiyo upewa wa Roho Mtakatifu sio mwanzo wa maisha mpya au maisha nyingine ya wokovu wetu. Apana. Lakini ni mwendelezo ya Mafundisho ya Yesu ambao aliwafundisha wale Mitume wake( na wafuasi wengine) ambao waliochaguliwa naye Yesu Mwenyewe kwa ajili ya uwenjilisaji wa Injili takatifu na ufalme wa Mungu dunia Kote.( tusome Mathew/Mathayo 28, 18-20). Kwa hiyo, Roho Mtakatifu ni mmoja katika ya zile nafsi tatu za Utatu Mtakatifu ambao katika umoja wao uendelea kulitakatifuza Kanisa na waamini wake siku hadi siku. Ndio maana Kanisa inatufundisha kama ifatavyo: Mwana wa Mungu, katika hali ya kibinadamu aliyofungamana nayo aliposhinda mauti kwa kifo na ufufuko wake, alimkomboa mwanadamu, akamgeuza kuwa kiumbe kipya.(tusome Gal. 6,15 na 2Cor. 5, 17). Maana kwa kuwashirikisha Roho wake, anawafanya ndungu zake waitwao kutoka katika mataifa yote kuwa mwili wake katika fumbo... (haya mafundisho tunayapata katika Konstitusio ya Kidogma juu ya Fumbo la Kanisa ukurasa wa 7)
Ndio sababu Injili yetu inatuonesha wazi kazi na Nguvu ya Mungu Roho Mtakatifu katika maisha ya Mitume na wafuasi wa kwanza wa Yesu pia katika maisha yangu na wewe leo. Mitume ambao walikuwa wakishikwa na hofu kubwa na manunguniko baada ya kifo cha Yesu Mwalimu na Kiongozi wao basi ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya wayahudi, akaja Yesu kuwapa amani na baadae akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana: akawavuvia, akawaambia, pokeeni Roho Mtakatifu kama ishara ya kuwapa tena uzima yaani uhai na nguvu ya kubaki imara katika kuamini kwao. Pia akawapa mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi yaani hapa tunaona mwanzo wa sakramenti ya Kitubio....
Katika somo la kwanza kutoka katika Matendo ya Mitume sura 2:1-11 tunasikia simulizi vile vile ya ujio wa Roho Mtakatifu kwa Mitume na wafuasi wengeni. Yaani ilikua katika hali hiyo ya sherehe na kusanyiko la mkutano huo mkubwa siku ya Pentecoste ya Kiyahudi, Mitume  kwa hofu ya Wayahudi walikuwa wamejifungia katika chumba, wakidumu katika kusali, wakisubiri ahadi ya Kristo, yaani ujio wa Roho Mtakatifu. Humo ndani ghafla kukaja upepo toka mbinguni,ukaijaza nyumba ile, zikatokea ndimi za moto zilizogawanyika zikiwakalia kila mmoja. Wote wakajawa Roho Mtakatifu, wakapata ujasiri wakatoka nje, wakaenda hekaluni kwenye kusanyiko wakaanza kuhubiri kwa nguvu habari za Yesu Kristo. Jambo la ajabu wanapata pia kipaji cha kuongea lugha geni. Kwa kuwa siku hiyo kwa sababu ilikuwa sherehe ya Pentecoste ya kiyahudi, wayahudi walitoka sehemu mbalimbali za dunia na kuelekea Yerusalemu kama desturi yao kwa ajili ya kusherekea pamoja, huku walijiufunza lugha mbalimbali lakini cha kushangazwa wakati Mitume baada ya kupokea Roho Mtakatifu walinena katika lugha mbalimbali nao walishangaa sana kuwaona Mitume wakiongea lugha ambazo zi na husiana na mataifa nyingine... lakini wote walikuwa kakielewana.
Basi wapendwa leo Kwetu sisi kwa ubatizo wetu tulipewa Roho Mtakatifu na katika sakramenti ya Kipaimara(confirmation) tunaimarishwa na Roho Mtakatifu na kutufanya kuwa askari hodari wa Kristo na wa Injili takatifu. Kwa hiyo Roho Mtakatifu ni Mungu kwetu ambaye anastahili sifa na shukrani kutoka kwetu. Akuna mwanadamu ambaye anaweza leo kujidai kuwagawiya wenzake wanadamu Roho Mtakatifu kama vile tunavyo sikia leo katika mafundisho mbalimbali katika dunia yetu ya leo. Basi ndugu zangu, ukisha batizwa basi tambuwa kwamba umebatizwa katika Kristo na Katika Roho Mtakatifu basi hauna tena budi ya kutafuta kupewa kwa namna ya pekee Roho Mtakatifu lakini ukiishi katika uaminifu na ukimwomba Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu wewe utapewa paji ao vipaji vya Roho ambao vitakusaidia kadiri ya uwezo wako kumtangaza Kristo na Injili yake ya ufalme wa Mungu.
Leo hii tunaangaika kwa sababu ya upungufu wa imani ambao umatufanya tutafute ishara, maarifu ao miujiza kusudi tutambuwe kwamba Roho huyu yupo kati yetu...hii ni imani usio na msingi wa Kristo imani ya kidunia ambao utupotesha wengi leo. Leo hii kwa jina la Roho Mtakatifu viongozi mbalimbali ya dini wanagawanyika hadi kuwatenga kondoo wa Mungu, kuharibu familia mbalimbali licha tu ya utabiri ambao hauwendani na mafundisho ya Roho huyu mabaye kwetu sisi ni Roho wa haki, ukweli, umoja na uzima. Basi kila mmoja wetu lazima afanye utafiti wa imani yake na kijipima kwamba kweli ndani mwaka Roho huyu anafanya kazi. Kila mmoja nivizuri ajiulize kwamba kweli ndani mwake anao vipaji vya Roho Mtakatifu ambao vinaweza kuwasaidia wengini kumfuata Kristo.
Ndio maana katika somo la 3 litokalo katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto sura 12: 3-7, 12-13 utukumbusha wazi kwamba: hatuwezi kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Ingawa kunatofauti ya karama, bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana... kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu wayahudi, au kwamba tu wayunani, ikiwa tu watumwa au tu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Paulo aliwakumbusha jumuiya ya Korinto na kutukumbusha leo kwamba sio vizuri kujisifia kwa mimi nilipewa vipaji muhimu kuliko wenzetu bali kujikweza na kufahamu kwa yote tunaoyatenda leo ni kazi yake Mungu ambao hutenda kupitia hekima ,akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu.Karama zingine ni kama vile unabii,Uponyaji, ualimu, kunena kwa lugha na nyingine nyingi ndani yetu basi sisi ni vyombo tu ambamo Mungu mwenyewe hutenda ishara yake. Basi tuwe wakweli na wanyenyekevu, tusiwadanganye wenzetu kwa kulitumia vibaya jina la Mungu Roho Mtakatifu.
Hivyo basi, yatupasa kutambua karama hizo zote ni mali yake Mungu. Leo hii kutokana na matatizo yatuzungukayo baadhi ya waamini wa Madhehebu mbalimbali, hata ndani ya Kanisa letu wanaonekana kukazia zaidi karama mbili tu yaani uponyaji na kunena kwa lugha. Roho Mtakatifu si fukara(poor au pauvre) wa vipaji,anavyo vingi sana kama vile hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu. Vipaji hivyo na vingine vingi ambavyo hatujavitaja vipo kwa ajili ya kuhudumiana na kujengana, yaani kwa lugha nyepesi ni kufaidiana sisi wenyewe. Yatupasa kuvitambua vipaji hivyo vyote kuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu. Tukumbuke kuwa imani inayotegemea miujiza tu haina nguvu, tena ni imani isiyo ya kweli. Aidha, kuna hatari kubwa ya kuingiza utapeli katika ile tudhaniyo kuwa ni miujiza. Vipaji tulivyonavyo viwe kwa manufaa ya wote. Na tujue kuwa karama kubwa kuliko zote ni upendo.
Na kazia tena nakusema: tunasherehekea ujio wa Roho Mtakatifu; siku ya Pentekoste, ambapo Roho Mtakatifu alionekana kuwashukia Mitume. Tusidhani kuwa Roho Mtakatifu alianza kuwepo siku ya Pentecoste: APANA! Yeye ni Mungu nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, hana mwanzo wala mwisho, ila tu siku ya Pentekoste alijidhihirisha kwa namna ya pekee. Tangu hapo yeye ni kiongozi wa kanisa kama vile ilivyokuwa amri za Mungu kwa taifa la Israeli. Wote wanaoshukiwa nae hujazwa mapaji yake saba ili tutende kazi ya Mungu. Hivyo, Roho Mtakatifu, ndiye anayeliongoza kanisa kuwachagua viongozi wa kanisa, kuwapeleka anakopenda wakafanye utume wao, anawajalia hekima katika utume na kuwasaidia katika maamuzi, anawasaidia wahubiri wa Injili kuhubiri vema, na kuongoza usomaji wa Maandiko Matakatifu.Tena Roho Mtakatifu huwajalia watu vipaji mbalimbali kwa ajili ya kanisa lote na kwa ajili ya wanakanisa wote,kwa ajili ya wokovu wa wote na kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.
Kwa hiyo wapendwa katika Kristo, sisi leo tuzingatiye mambo muhimu mbili tunapo sherekeya siku hii ya Petencoste: kwanza tukumbuke kuwa Roho Mtakatifu anakuja bado kwetu katika sakramenti ya Ubatizo na Kipa-imara(confirmation). Roho huyo hutujalia vipaji mbalimbali. Tuzikimbilie sakramenti hizo na tutumie vema vipaji vyetu tulivyojaliwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya kufaidiana: kwa hiyo tusiwe na majivuno kwa sababu ya vipaji tulio pewa, tuheshimu vipaji vya wenzetu pia tusiwe na vivu mbaya kwa vipaji vya wenzetu sisi sote tulipewa vipaja tofauti kwajili ya kazi Ya Mungu sio kwa ajili ya kazi yetu. Pili, tudumishe umoja katika kanisa, sio sisi na Yesu Kristo tu bali hata sisi kwa sisi. Muujiza wa Pentekoste ulirudisha umoja uliopotea huko kati ya mataifa: Muujiza huu uwe mfano wa utume wetu katika dunia yote bila ubaguzi wa rangi, jinsia, kabila, utaifa, ukanda, ujimbo etc., ili watu wote wapate kulisikia Neno la Mungu, ili wapate kuliishi na kuokoka: kama wabatizwa yatupasa kuongea lugha moja tu, lugha ya upendo kwa wote, lugha ambayo hakuna asiyeielewa. Upendo haufifii kamwe kwani wadumu mpaka Mbinguni. Ni fadhila ya Kimungu iliyotofauti na nyingine kwani mwisho wake si hapa Duniani. 

SHALOOM: MUNGU AWABARIKI KILA SIKU YA MAISHA YENU

SHEMASI BIENVENU KABEYA NGUNGWA KUNGWA POULAIN LOQUACE, SDS

Commentaires

Posts les plus consultés de ce blog

MAHUBIRI YA SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU MWAKA A WA KANISA: ATUKUZWE BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU, MUNGU AMBAYE YUPO, ALIYEKUWAKO, NA ATAKAYEKUJA

MAHUBIRI YA ADHIMISHO YA ALHAMISI KUU TAKATIFU : EKARISTI NI ALAMA YA UPENDO NA UMOJA