MAHUBIRI YA DOMINIKA YA MATAWI MWAKA A WA KANISA


DOMINIKA YA MATAWI AO DOMINIKA YA MATESO MWAKA A

MASOMO

Somo I:Isa. 50:4-7.
Somo II:Flp. 2:6-11.
Injili: Mt.  26:14-27:66


SALA: Ee Bwana tunakushukuru kwa wema na upendo wako mkuu kwa kumtoa Mwanao Mpendwa Yesu Kristu kuwa sadaka kwa ajili ya wokovu wetu basi e Bwana tunakukabidhi watu wanaoteseka na ugonjwa wa virusi vya Korona: Ee Mungu Baba yetu pokea marehemu wote kaika ufalme wako.

UFAFANUZI WA DOMINIKA YA MATAWI
Ndugu zangu katika Kristo, tangu jumatano ya majivu tulianza kipindi cha Kwaresima kipindi ambacho Mama Kanisa anatualika kututafakari kwa kina mafumbo ya wokovu wetu. Katika kipindi hiki tunaungana na Yesu katika safari yake ya ukombozi, kwa kufunga, kusali na kutenda matendo ya huruma kwa maskini, wanyonge na jirani zetu. Basi leo Mama Kanisa anahadhimisha Dominika ya Matawi dominika amboyo inatuingiza taratibu katika kilele cha imani na matumaini yetu kusudi tukumbuke na kutafakari pamoja lile fumbo la Pasaka la Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Wapendwa, Dominika ya leo inasehemu kuu mbili. Katika sehemu ya kwanza  tunakumbuka kuingia kwa shangwe Bwana wetu Yesu Kristo katika mji wa Yerusalemu, akishangiliwa kama Mfalme na Masiha, na katika sehemu ya pili tunakumbuka Mateso na Kifo ya Bwana wetu Yesu Kristo Msalabani.

Wapendwa, leo Yesu Kristo anaingia kwa shangwe na furaha katika mji wa Yerusalemu huku tukichukua matawi na kutandika nguo zetu tukimtangaza kwamba ndiye Masiha na Mfalme. Katika liturgia ya Kanisa matawi ni ishara ya ushindi na matumaini kwa Masiha: na hayo tunayapata katika utamaduni wa wayahudi baada ya kupata ushindi walisherekeya wakichukua fimbo zilizopambwa majani, na matawi, na majani ya mitende, wakipaza nyimbo za shukrani kwake Yeye aliyewafanikisha na kuwawezesha kupatakasa mahali pake penyewe.(cfr. 2Wamakabayo 10: 6-7) Pili kuingia kwa utukufu kwake Bwana wetu Yesu Kristo ni hitimisho ya utabiri wa manabii katika agano lakale hususani kutimia kwa utabiri wa nabii Zekaria aliye tabiri ujio wa Masiha wa Israeli ambaye ni mnyenyekevu na wa amani akisesma “Furahi sana ee binti Sayuni, piga kelele ee binti Yerusalemu! Tazama mfalme wako anakuja kwako. Ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana punda, mtoto wa punda” (Zek.9:9).
Basi wapendwa sisi leo tunakusanyika hapa kwanza kumshukuru Mungu yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kwa Upendo wao mkuu kwetu na pia kumshangilia Yesu Kristo Masiha na Mfalme wetu ambaye kwa Utii na Unyenyekevu wake akatwaa namna ya mtumwa, akawa mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam ya msalaba kwa ajili wa wokovu wetu na wa dunia nzima: kwa hiyo kwa shangwe na kuimba tumtukuze na kumshangilia nakusema: hosanna, hosanna juu mbinguni.

UFAFANUZI WA MATESO YA BWANA 
Wapendwa katika Kristo, Matukio haya mawili ya Dominika ya leo yanatuonesha wazi hali alisi, hisia, tabia maisha yetu sisi wanadamu: wale walikuwa wakibeba matawi mikononi, wakitandaza nguo zao, wakiimba hosanna mfalme wetu... baadaye wanakuja tena na kupiga kelele: asulibiwe. Basi wazo hili la kukamatwa Yesu linatuingiza wazi katika sehemu inayodokeza msingi wa pili wa Dominika ya leo. Kwanza tujiulize kwa nini Yesu auwawe ili sisi tuokolewe? Nani alimuhuwa Yesu? 

Wapendwa kanisa linatufundisha kwamba kifo kikatili cha Yesu hakikuwa tukio lisilotakiwa, ambalo limetokea kwa bahati mbaya, kwa kuingiliana na mazingira yasiyotakiwa, bali ni sehemu ya fumbo la mpango wa Mungu. Na mtume Petro baada ya kujazwa na Roho Mtakatifu aliwahubiria wayahudi wa Yerusalemu akisema: Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya Yesu wa Nazareti mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua, mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa.(Cfr. Mdo 2:23 na KKK 599) ndio maana Kanisa linahimiza sana kwamba utata wa kihistoria wa kumhukumu Yesu wadhihirika katika masimulizi ya Injili. Dhambi yoyote ile ya binafsi ya wahusika wakuu anaijua Mungu peke yake. Hivyo hatuwezi kuwahesabia hatia wayahudi wote wa Yerusalemu kwa jumla.(Cfr.KKK597).
Basi wapendwa wenye dhambi wote, walikuwa chanzo cha Mateso na Kifo ya Yesu. Na leo hii kila mja wetu mwenye dhambi ni kweli sababu na chombo cha mateso ya mkombozi wetu. Basi ya muhimu leo ni kwamba Je, mimi na wewe tunayatazamaje mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na mateso yetu ya kibinadamu? Leo hii maisha yetu yamejaa na mateso ya kila hina vita, njaa, maradhi, ya kiafya kama corona virus lakini je mateso haya tunayaelewa namna gani? Na je tunayapokea kwa imani?  Je, msalaba unamaana gani kwangu, kwako leo? 

Bila shaka Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo ni ushindi dhidi ya mahangaiko, woga, shida na mashaka mbalimbali ya maisha yetu. Kwa hakika mateso haya ya Yesu Kristo yanaimarisha na kuchochea imani yetu hasa tukikumbuka kuwa hakuna  utukufu pasipo mateso; mateso na utukufu vinaambatana pamoja. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yabadili muono na mtazamo wakibinadamu, kwani Yesu hatishwi na chochote anakwenda Yerusalemu huku akijua itampasa kukamatwa na kuteswa ili atukomboe mimi na wewe wadhambi. Yesu anajua kwa hakika thamani ya roho zetu ndio maana kuteswa, kutemewa mate, kupigwa mijeledi na kuchomwa ubavu kwa mkuki kwake hayo si kitu ila roho yako na yangu zipate kupona. Kwa upendo wake kwetu ameamua kuuacha utukufu na kuishi maisha duni ili atukomboe kupitia njia hii ya msalaba.

Basi wapendwa msalaba kwetu ni ishara ya ushindi, ishara ya umoja, ni ishara ya upendo ambao hauwezi kwesabika: kwa hiyo sisi kama wafuasi wake inatupasa kuisha katika umoja, katika kuvumiliana na katika unyenyekevu. Labda msalaba wako ni uwongo na majungu katika jumuiya, labda msalaba wako ni utamaduni na mila na desturi yako katika jumuiya yetu, labda wewe ni zarawu na kuwahonea wengine… lakini Yesu anatuku,busha mimi na wewe leo kuwa sadaka kwa wenzentu huku tukisaidiana kama jumuiya pamoja kuchugua misalaba yetu na kuyapeleka kwa Yesu. Lakini kumbuka, kama mateso haya tunayapokea kwa imani yanathamani kubwa, kwani tutayapokea kwa uvumilivu, upole na kwa kuwajali wale wote wanaoteseka na kwa mateso hayo tutapata faida zaidi kiroho na kimwili. 
Wapendwa katika Kristo, tumwombe Mungu atujalie moyo thabiti na wa ujasiri wa kuyapokea mateso kama Kristo katika maisha yetu ili yatuimarishe na kutunganisha zaidi na Kristo aliyevumilia mateso kwa ajili ukombozi wetu.

Shemasi Bienvenu Kabeya Ngungwa Kungwa Poulain Loquace, SDS


Commentaires

Posts les plus consultés de ce blog

MAHUBIRI YA SHEREHE YA PENTEKOSTE MWAKA A WAKANISA: ROHO MTAKATIFU HULITAKATIFUZA KANISA

MAHUBIRI YA SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU MWAKA A WA KANISA: ATUKUZWE BABA NA MWANA NA ROHO MTAKATIFU, MUNGU AMBAYE YUPO, ALIYEKUWAKO, NA ATAKAYEKUJA

MAHUBIRI YA ADHIMISHO YA ALHAMISI KUU TAKATIFU : EKARISTI NI ALAMA YA UPENDO NA UMOJA